Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Programu hii ilifanyika kwa ushiriki wa wanazuoni wa Kishia na Ahlu Sunna, wahadhiri wa vyuo vikuu, wanafunzi pamoja na watu wenye kuvutiwa na masuala ya umoja wa Kiislamu. Katika hafla hiyo, Mheshimiwa Haji Hemmat-Panah, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania, Profesa Khalifa Khamis, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kundecha, Mwenyekiti wa Maimamu wa Swala ya Ijumaa na Jamaa, Dkt. Ali Dina, Sheikh Ali Saalim utoka Kenya pamoja na Mkurugenzi wa Ofisi ya uwakilishi wa Jamiat al-Mustafa nchini Tanzania walitoa hotuba.
Mwakilishi wa Jamiat al-Mustafa, katika sehemu ya hotuba yake huku akisisitiza umuhimu wa tukio la Ghadir alisema: “Ghadir Khum ni moja ya matukio makubwa zaidi katika historia ya Uislamu; tukio ambalo halikupokelewa tu katika vyanzo vya Kishia, bali pia limenukuliwa katika vyanzo vya kuaminika zaidi vya Ahlu Sunna, na asili ya kutokea kwake ni jambo linalokubaliwa na Waislamu wote. Hadithi tukufu isemayo: “مَنْ كُنْتُ مَوْلَاهُ فَعَلِيٌّ مَوْلَاهُ” ni miongoni mwa Hadithi mutawatir za Kiislamu ambazo zimeandikwa katika vyanzo mbalimbali vya Kishia na Ahlu Sunna.”
Aliongeza: “Ingawa Shia na Ahlu Sunna wana mitazamo tofauti kuhusu tafsiri ya maana ya neno Maula, lakini wanakubaliana kuhusu ubora, utukufu, hadhi na mapenzi kwa Amirul-Mu’minin, Mtukufu Ali bin Abi Talib (a.s), na humtambua kuwa mmoja wa watu mashuhuri zaidi katika historia ya Uislamu na mfano wa uadilifu, uchamungu na imani.”
Mkurugenzi huyo, akielezea umuhimu wa kuimarisha umoja wa Kiislamu, alibainisha: “Ghadir inaweza kuwa, badala ya kuwa chanzo cha tofauti, sehemu ya mazungumzo, kujuana na kuimarisha udugu wa Kiislamu. Leo Umma wa Kiislamu unahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote mshikamano, umoja na ushirikiano, na Qur’ani Tukufu pia inawahimiza Waislamu kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na mifarakano.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alizungumzia pia shakhsia na fikra za Mtukufu Imam Khomeini (r.a) na kusema: “Imam Khomeini (r.a) aliona umoja wa Umma wa Kiislamu kuwa ni miongoni mwa misingi muhimu ya fikra zake za kisiasa na kidini, na daima alisisitiza mambo yanayowaunganisha Waislamu. Kutangaza Wiki ya Umoja na juhudi za kuleta ukaribu baina ya madhehebu ya Kiislamu ni miongoni mwa turathi zake za kudumu katika ulimwengu wa Kiislamu.”
Katika mkutano huu, wazungumzaji walieleza vipengele mbalimbali vya tukio la Ghadir na kusisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kielimu kati ya madhehebu za Kiislamu, kuimarisha maisha ya pamoja kwa amani, kupambana na misimamo mikali na kutumia uwezo wa mambo ya pamoja ya Waislamu katika kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu.
Miongoni mwa mandhari za kiroho na zenye athari kubwa katika hafla hiyo ilikuwa ni kuingizwa kwa bendera iliyobarikiwa ya Amirul-Mu’minin, Mtukufu Ali (a.s), na mmoja wa watumishi wa Ahlu Bayt (a.s) katika eneo la hafla hiyo, jambo ambalo lilifanya mazingira ya mkusanyiko huo kuwa ya kiroho zaidi na yenye nuru zaidi, na likapokelewa kwa heshima na mapokezi maalumu kutoka kwa waliohudhuria. Washiriki walionyesha mapenzi yao kwa hadhara takatifu ya Bwana wa wachamungu (a.s), na waliipokea programu hiyo ya kiroho kwa furaha huku wakiiita pambo la mkutano huo wa kielimu na kitamaduni.
Mkutano huu ulifanyika katika mazingira ya kirafiki, ya kielimu na yenye kujenga umoja, na washiriki walisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanyika kwa programu kama hizi kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa Umma wa Kiislamu, kueneza utamaduni wa mazungumzo na kuimarisha uelewano wa pamoja kati ya wafuasi wa madhehebu ya Kiislamu.


Maoni yako